Hossein Amir- Abdollahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria ziara ya Rais Ebrahim Raisi huko Syria na akasema umuhimu wa ziara hii katika nyuga za kisiasa, kiusalama na kiuchumi unadhihirisha ushindi wa irada ya kisiasa ya muqawama na kufanikiwa diplomasia ya serikali katika kukamilisha mchakato wa ushirikiano wa kikanda.
Rais Sayyid Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo Jumatano anaelekea Syria akiongoza ujumbe wa ngazi ya juu wa viongozi wa kisiasa na kiuchumi kufuatia mwaliko rasmi wa Rais wa nchi hiyo Bashar al Assad. Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na ujumbe aliofuatana nao katika ziara hiyo ya Syria; wakiwa nchini humo katika ziara ya siku mbili watakutana na kuzungumza na viongozi wa ngazi ya juu wa nchi hiyo kuhusu njia mbalimbali za kukuza na kuimarisha uhusiano wa kisiasa na kupanua viwango vya ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya pande mbili.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aidha atabadilishana mawazo kuhusu namna ya kupanua ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara baina ya nchi mbili atakapozungumza na waandishi wa habari. Kukutana na kuzungumza na raia wa Iran wanaoshi Syria na pia kuzuru maeneo matakatifu nchini humo ni kati ya ratiba nyingine katika ziara ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huko Syria. Hii ni ziara ya kwanza kufanywa na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huko Syria baada ya kupita miaka 13.
342/